Kila Mei 28, duniani kote wadau wa afya na jinsia huadhimisha siku ya hedhi duniani. Shirika la WaterAid Tanzania liliungana pamoja na wanafunzi na walimu katika shule ya Misima iliyoko halmashauri ya mji wa Handeni katika hafla ya kukabidhi mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji na mafunzo tabia siha uliofadhiliwa na shirika la Hilton Global Foundation pamoja na WaterAid ili kupunguza makali ya ukosefu wa maji katika shule hiyo hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika kipindi cha hedhi.
Sambamba na ukarabati wa huduma za maji na tabia siha, Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania Bi Anna Mzinga alimkabidhi mkuu wa shule cherehani moja kwa ajili ya wanafunzi kujishonea pedi za kitambaa, vifaa 40 vya kushonea pedi, katoni 55 za pedi (kutumika katika kipindi cha mvua pale pedi za kufua zitashindwa kukauka), vifaa vya michezo seti 3, mabango 20 kwa ajili ya kujifunza masuala ya usafi na televisheni kwa ajili ya kujifunza tabia siha na usafi kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkuu wa WaterAid Tanzania BI.Anna Mzinga akimkabidhi vifaa mbalimbali Afisa Tawala Bi.Upendo Magashi kwa ajili ya Shule ya Sekondari Misima
Bi. Anna Mzinga alisema: “tumefanikisha ukarabati wa miundombinu kadhaa ya mfumo wa maji, matenki la kuhifadhia maji, vyoo ikiwemo kuweka muundombinu wa choo rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na zaidi ya yote kutoa elimu kuhusu usafi kwa wasichana na wavulana katika hatua za makuzi yao binafsi hii ilijumuisha mafunzo maalumu ya namna ya kujitengezea taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi ili kujilinda na adha mbalimbali wanapokua katika kipindi cha hedhi.”
Akiongea katika hafla hii Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Handeni Ndg Upendo Magashi alisisitiza: “ Miundombinu hii inahitaji kutunzwa ili iweze kutoa huduma husika kwa kipindi kirefu kwa sasa na kwa wanafunzi watakaokuja kusoma katika shule hii hivyo haina budi itunzwe”
Afisa Tawala Bi.Upendo Magashi, akikabidhi vifaa mbalimbali kutoka WaterAid Tanzania kwa walengwa, ambao ni wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Misima
Licha ya kwamba jitihada za dhati zimefanyika na serikali pamoja na wadau ila bado inaripotiwa kwamba 34% ya wasichana hukosa vipindi shuleni kutokana na upungufu wa vyumba maalumu vya kujisitiri wakati wa hedhi huku 26% kutokana na ukosefu wa maji na vyoo safi katika shule.
Kauli mbiu ya kitaifa ya siku ya hedhi inasema “Hedhi ni tunu na Msingi wa Afya kwa wasichana na Wanawake, Tuiwezeshe"
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.