Baraza Maalum la Madiwani la Halmashauri ya Mji Handeni limependekeza kuongezwa kwa maeneo ya utawala katika Jimbo la Handeni Mjini kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii, kiuchumi na miundombinu kwa wananchi.
Katika kikao kilichofanyika tarehe 14 Machi, 2025 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Handeni, madiwani wamependekeza kuongezwa kwa kata sita kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Kata hizo ni Kang'ata, Kiva, na Kwaluguru zilizo mashariki mwa Halmashauri zenye wakazi 46,220, pamoja na Misima, Sideni, na Kwamatuku zilizo kaskazini mwa Halmashauri zenye wakazi 58,227.
Aidha, Maeneo haya yamependekezwa kutokana na jiografia yake, kwani wakazi wake wanategemea huduma mbalimbali za kiuchumi, kijamii na miundombinu kutoka Halmashauri ya Mji Handeni.
Kikao hiki kilihudhuriwa na wakuu wa idara na vitengo, watendaji wa kata, wawakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama. Baada ya majadiliano, baraza limeazimia kuwa maeneo hayo yaongezwe katika Jimbo la Handeni Mjini ili kuimarisha usimamizi wa maendeleo ya wananchi.
Hatua hii inasubiri maamuzi ya mamlaka husika kwa utekelezaji rasmi wa pendekezo hilo.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.