Na Augusta Njoji, HANDENI TC
“Zamani tulikuwa tunaamka alfajiri na kutembea umbali mrefu, lakini sasa ndoto zetu ziko karibu na nyumbani,” anasimulia kwa tabasamu mwanafunzi Saidi Mkomwa, akielezea mabadiliko makubwa yaliyoletwa na ujio wa shule mpya katika eneo lao.
Kwa Saidi na wanafunzi wenzake, kufunguliwa kwa Shule ya Sekondari ya Amali Mapinduzi iliyopo katika Halmashauri ya Mji Handeni, mkoani Tanga, si tukio la kawaida bali ni hatua muhimu iliyobadili maisha yao ya elimu na matarajio ya baadaye.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule 103 za Sekondari za Amali nchini zilizojengwa kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) unaoratibiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shule ya Sekondari ya Amali Mapinduzi ndiyo ya kwanza ya Sekondari ya Amali ya Mkondo wa Kilimo katika Halmashauri hiyo, mradi uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 584.2.
Ujenzi wa shule hiyo umelenga kutoa elimu yenye mwelekeo wa vitendo, hususan katika fani ya kilimo, ili kuwaandaa vijana kuwa wabunifu, wenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao ya sekondari.
Miundombinu iliyopo shuleni hapo imejengwa kwa viwango vya kisasa, ikijumuisha madarasa, maabara, mabweni, nyumba za walimu, ofisi pamoja na miundombinu ya umeme, hatua inayolenga kuweka mazingira rafiki na salama ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla ya ujenzi wa shule hiyo, Saidi Mkomwa anasema wanafunzi walikumbwa na changamoto kubwa ya umbali kufuata elimu katika shule mbalimbali za sekondari katika Mji huo.
“Tulikuwa tunatembea takribani kilometa 22 kwa siku kwenda na kurudi shule ya sekondari. Ilikuwa ni safari ngumu, ya kuchosha na wakati mwingine ilituathiri hata katika masomo,” anasema.
Naye, Asha Somboja, mwanafunzi mwingine, anakiri kuwa umbali huo ulikuwa kikwazo kikubwa kwao.
“Wakati mwingine nilichelewa vipindi kwa sababu ya uchovu wa kutembea umbali mrefu. Sasa shule ipo karibu na makazi yetu, tunasoma kwa amani, tukiwa na nguvu mpya,” anasimulia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Amali Mapinduzi, Projectus Maula, anasema shule hiyo tayari imeanza kupokea wanafunzi Septemba 2025 kutoka maeneo ya karibu, huku maandalizi yakiendelea kupokea wanafunzi kutoka maeneo ya mbali zaidi kutokana na upekee wake kama shule ya amali.
“Hii ni shule ya amali ya kilimo. Masuala ya kilimo yatafundishwa kwa vitendo, na siku si nyingi maabara ya kilimo itajengwa. Tunashukuru Serikali kwa kuajiri walimu na kuruhusu shule hii kuanza mapema,” anasema.
Anabainisha kuwa ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu, kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kuhakikisha vijana wanapata stadi zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Serikali, Mpango wa SEQUIP ulianzishwa kwa lengo la kuboresha ubora wa elimu ya sekondari nchini kwa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wa kike na wa kiume, pamoja na kuwaandaa vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya Taifa.
Kupitia mpango huo, Serikali imejikita katika ujenzi wa shule za kisasa za amali, maabara, mabweni, nyumba za walimu, pamoja na kuajiri na kuwajengea uwezo walimu, huku mkazo ukiwekwa katika elimu ya vitendo ili vijana waweze kujitegemea.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.