Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni imezindua rasmi Kampeni ya “Catch-Up” yenye lengo la kuimarisha juhudi za kutambua na kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu. Kampeni hii inalenga kugundua wagonjwa wapya 99 wa kifua kikuu ndani ya mwaka, kwa kuhakikisha uchunguzi wa mapema na matibabu sahihi kwa wagonjwa wanaogundulika, ili kupunguza maambukizi mapya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hii, Bwana Jonas Mkondya kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni alisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja katika kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu, ambao takwimu zinaonyesha kuwa mgonjwa mmoja wa kifua kikuu cha mapafu ambaye hajagunduliwa anaweza kuambukiza watu takriban 10 ndani ya mwaka mmoja.
Kampeni hii inalenga makundi yaliyo hatarini zaidi, ikiwemo watoto wanaoishi na wagonjwa wa kifua kikuu, watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (VVU), wafungwa, na watu wanaoishi katika maeneo yenye msongamano kama machimboni na masokoni. Katika Halmashauri ya Mji Handeni, maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kideleko, Kwedigongo, Kwaluwala, Msaje, Zizini, na Bwila.
Huduma za uchunguzi wa kifua kikuu zinapatikana katika Hospitali ya Mji Handeni, Kituo cha Afya Kideleko, na Zahanati ya Msekwa, ambapo teknolojia kama GeneXpert, TruNat, mionzi ya X-ray, na dadubini hutumika. Hata hivyo, sampuli kutoka maeneo mengine bado husafirishwa hadi vituo hivi kwa ajili ya uchunguzi.
Takwimu za UgonjwaKwa wastani, Halmashauri ya Mji Handeni hugundua wagonjwa 130 wa kifua kikuu kila mwaka. Kwa sasa, kuna wagonjwa 74 walioko kwenye matibabu, mmoja kati yao akiwa ni mgonjwa wa kifua kikuu sugu.Halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huu, ikiwemo chanjo ya BCG kwa watoto wachanga, tiba kinga kwa watoto chini ya miaka 5 na wagonjwa wa VVU, pamoja na utoaji wa elimu kuhusu kifua kikuu katika vituo vya afya na mashuleni.
Kwa kushirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kampeni hii itahakikisha inafikia maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masoko, machimboni, shule za bweni, minadani, na kupitia ufuatiliaji wa nyumba kwa nyumba.Uzinduzi huu umeonyesha dhamira ya dhati ya Halmashauri ya Mji Handeni ya kuimarisha afya ya jamii kwa kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu kupitia ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali. Kampeni hii ni hatua muhimu katika kupunguza ugonjwa wa kifua kikuu katika Handeni Mjini.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.