Leo Tarehe 08/03/2023 Halmashauri ya Mji Handeni, imeadhimisha siku ya wanawake duniani yenye kauli mbiu ”UBUNIFU WA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA:CHACHU KATIKA KULETA USAWA WA KIJINSIA”, katika kata ya Konje, mtaa wa Konje shule, ghafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, waheshmiwa madiwani, watumishi kutoka Halmashauri ya Mji Handeni, wadau wa maendeleo ya jamii(CAMFED) na wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju na Mhe.Amina Kigoda Diwani viti maalum, wakijumuika na wananchi waliojitokeza katika kusherehekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Akizungumza katika hafla hiyo mwenyekiti wa Halmashauri(Diwani) wa kata ya Kwamagome Mhe.Mussa Mkombati ambaye ni mgeni rasmi, amempongeza mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju kwa namna anavyoweza kusimamia kama mtendaji mkuu wa Halmashauri, kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya kina mama, vijana na walemavu, pia amewataka walionufaika na mikopo wafanye marejesho kwa wakati ili wengine waendelee kunufaika na mikopo hiyo, Mhe.Mussa Mkombati aliendelea kwa kuwapa rai wakinamama wajitokeze Halmashauri ya mji Handeni na kuomba mikopo isiyo na riba na kuepuka kuchukua mikopo kwenye taasisi zenye masharti magumu, pia amewasisitiza wazazi kuwapeleka watoto shule hasa watoto wa kike ambao wanaathirika sana na changamoto ya kutopelekwa shule, kwani kushindwa kuwasimamia watoto kupata haki zao ndio sababu inayopelekea uharibifu wa maadili na hatimaye mimba za utotoni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni(Diwani) kata ya Kwamagome Mhe.Mussa Mkombati, akimzawadia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju kwa utendaji kazi wake uliotukuka, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Nae mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju, akizungumza na wananchi waliojitokeza katika hafla hiyo, ameendelea kuwahamasisha wakina mama wajiunge na vikundi ili kuweza kupata fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Mji Handeni, na pia amewashauri walionufaika na mikopo hiyo watumie pesa hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuweza kufanya marejesho kwa urahisi na kufikia malengo ya kujikwamua katika hali zao za kiuchumi, pia amewataka wazazi kutenga muda wa kuwasimamia na kufuatilia mienendo ya watoto wao wakike na wakiume ili kukabiliana na uharibifu wa maadili unaotokea katika jamii.
Katika hafla hiyo Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Mji Handeni, Ndugu.Fred Mpondachuma amewasisitiza wazazi kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata elimu wanapelekwa shule ili waweze kupata haki yao ya msingi ya elimu, pia amewataka wakina baba wawapatie fursa wakina mama katika kushiriki masuala yote ya kijamii bila kuwaacha nyuma na kuthamini michango yao katika jamii, Ndugu.Fred Mpondachuma amewaasa wazazi kutowaozesha watoto wao waliokuwa na umri mdogo ili kudhibiti ndoa za utotoni ambazo zinamkwamisha mtoto wa kike kutimiza ndoto zake. Na amewataka wanakikundi kufuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuwa na barua kutoka ofisi ya mtendaji pindi wanapofuatilia mikopo ili kuepusha kuchelewa kwa kupata mikopo hiyo.
Wadau wa maendeleo ya jamii Campaign for Female Education(CAMFED) wakitoa msaada kwa wanafunzi wa kike shule ya sekondari Konje, katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika Halmashauri ya Mji Handeni
Nae mkazi wa kata ya Konje Bi.Graciana Shirima, ametoa shukrani kwa Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dokta.Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele wanawake hususani katika suala la mikopo wanayoipata, ambayo imeweza kuwasaidia watoto katika afya, elimu na mahitaji mbalimbali ya kila siku, pia ametumia fursa hiyo kuhamasisha wanawake ambao hawajachukua mikopo, kuwa mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri ya Mji Handeni, haina riba na ni haki yao hivyo wajitokeze kwenye fursa hiyo, na kutumia mikopo hiyo pindi wanapoipata kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.