Uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya vibaoni uliofanyika leo tarehe 17-12-2022 umetamatika kwa wananchi wa kata ya vibaoni yenye mitaa mitano(5) na vituo 12 vya kupigia kura, kumchagua Ndugu. Marry Mntambo Chambuya(CCM) kuwa diwani mteule wa kata ya vibaoni kwa kura 1400 dhidi ya mshindani wake Ndugu Hilaly Seif Kitwanga wa chama cha wananchi CUF aliyepata kura 214.
Akitangaza matokeo hayo ya uchaguzi mdogo wa kata ya vibaoni kwenye ofisi za kata ya vibaoni, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Bi. Zainabu Mhanga amesema jumla waliojiandikisha kupiga kura ni 4186, waliopiga kura ni 1654 , kura halali ni 1614 na kura zilizoharibika ni 40.
Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya vibaoni Bi. Zainabu Mhanga akitangaza matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya vibaoni mbele ya wananchi waliojitokeza kusikiliza matokeo hayo kwenye ofisi za kata ya vibaoni.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa matokeo hayo, mshindi wa uchaguzi huo mdogo wa udiwani Bi. Marry Chambuya amewashukuru wapiga kura wote waliojitokeza siku ya leo, wasimamizi wa uchaguzi, na viongozi mbalimbali walioshiriki katika zoezi zima la uchaguzi. Ameahidi kuwa kiongozi wa wananchi wote wa kata ya vibaoni bila ubaguzi wa aina yoyote.
Nae msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Handeni mjini ambae pia ni Mkurugenzi wa Halmshauri ya mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju, amewashukuru wananchi wa kata ya vibaoni kwa kujitokeza na kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura na kumchagua diwani wa kata yao katika hali ya utulivu na amani. Pia amewashukuru viongozi wa ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya kulinda amani kipindi chote cha kampeni, siku ya kupiga kura mpaka wakati wa kutangazwa kwa matokeo.
Msimamizi mkuu wa Uchaguzi wa Jimbo la Handeni Mjini ambae pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Handeni Bi. Maryam Ukwaju akizungumza na wananchi waliojitokeza mara baada ya matokeo kutangazwa.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mji Mh. Mussa Mkombati(Diwani CCM) amesema ameupokea ushindi wa Bi.Marry Chambuya kwa furaha kubwa huku akisema kuwa hayo yametokana na matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali inayoongozwa na CCM chini ya Rais wake Daktari Samia Suluhu Hassan, ambapo amempongeza diwani mteule kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa kata ya vibaoni na amemuahidi ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwake na Baraza zima la madiwani wa Halmashauri ya mji Handeni.
Na mwandishi wetu
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.