Leo tarehe 03/03/2023 Halmashauri ya Mji Handeni imetoa jumla ya shilingi milioni 63,665,300 kwa vikundi vya wajasiriamali mbalimbali wa Halmashauri ya mji Handeni fedha zinazotakana na asilimia kumi ya mapato ya ndani katika ghafla fupi iliyofanyika katika eneo la Bomani, mahali ilipo ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Handeni.
Akizungumza mbele ya Mgeni rasmi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Fred Mpondachuma alisema fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya mji Handeni katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyoanza mwezi wa 10 hadi mwezi wa 12, ambapo mikopo hiyo ni maalumu kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu huku akitaja jumla ya vikundi 18 vilivyoomba na kukidhi vigezo kunufaika na mkopo huo, amesema vikundi vya wanawake vipo 9, vikundi vya vijana vipo 6 na vikundi vya watu wenye ulemavu vipo 3. Bw. Mpondachuma amesema milioni 63 zilizotolewa mkopo siku ya leo zina mchanganuo ufuatao, milioni 42 zimetokana na 10% ya pato la ndani la Halmashauri na milioni 21 ni fedha zilizokusanywa kutoka kwenye marejesho ya waliokopeshwa hapo kabla.
Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya Mji Handeni Ndugu. Fred Mpondachuma akikabidhi taarifa fupi kwa Katibu Tawala wilaya ya Handeni Mh. Mashaka Mgeta wakati wa ghafla ya ugawaji mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bi.Maryam Ukwaju amemueleza mgeni rasmi kuwa mpaka kufikia sasa Halmashauri imeshatoa zaidi ya milioni mia moja na nne ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya mji Handeni kwa ajili ya mikopo hiyo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Amesema, Halmashauri inaendelea kukusanya vizuri na mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha mwezi Juni 2023 Halmashauri itakuwa imefikia zaidi ya asilimia 100 katika utoaji wa mikopo hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi. Maryam Ukwaju akizungumza mbele ya mgeni rasmi, hayupo pichani
Mgeni rasmi katika ghafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh. Alberto Msando amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti Mh.Mussa Mkombati na Mkurugenzi wake Mh.Maryam Ukwaju kwa kutimiza ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia wajibu huo wa kisheria. Amewahakikishia ya kwamba, atasimamia kikamilifu kuhakikisha uwezeshaji huu wa kiuchumi unakwenda kuwa na tija kwa kila mnufaika ili waweze kukua kiuchumi kwa haraka Zaidi. Amewatahadharisha wanufaika hao ya kwamba katika fedha walizokopeshwa, haitapotea hata shilingi moja katika kipindi chote atakachohudumu katika nafasi ya Mkuu wa wilaya ya Handeni, hivyo basi endapo kuna mtu amejiunga kwenye kikundi akifikiri mara baada yakukabidhiwa mkopo atakwamisha wengine kufanya marejesho, basi ni vyema akajitoa mapema kwenye kikundi hicho. Amewasihi wanakikundi, kusimamia katiba yao, kutunza amani na kuepuka mivurugano itakayopelekea wao kushindwa kutimiza lengo la kuchukua mkopo huo. Kwa upande wa waliochukua mkopo wa vyombo vya usafiri, amewataka kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka kukamatwa na pikipiki kuzuiliwa hali itakayopelekea kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati na kujiondolea sifa za kuendelea kukopesheka.
Wanufaika wa mikopo Halmashauri ya mji Handeni wakimsikiliza mgeni rasmi Mh. Alberto Msando, Mkuu wa wilaya ya Handeni.
Akizungumza mara baada ya kupokea mkopo kwa niaba ya wanakikundi wengine waliopokea mkopo wa pikipiki, mwanakikundi Ibrahim Mrisho Bakari dereva bodaboda wa Kata ya Chanika, amesema wamepokea mkopo huo kwa furaha sana, na wanamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwasababu pikipiki walizokopeshwa zitawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuwasogeza mbele kimaisha kwani bodaboda ni ajira halali na inaingiza kipato kinachowafanya wakidhi mahitaji yao ya kila siku, aidha Bwana Ibrahim ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza na kuchangamkia fursa kwenye Halmashauri zao ili waweze kupatiwa mikopo hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh. Alberto Msando akimkabidhi Bajaji Bw.Mhina Omari Mahimbo katika ghafla ya utoaji mikopo
Nae Bw.Mhina Omari Mahimbo aliyepatiwa mkopo wa pikipiki ya magurudumu matatu maarufu Bajaji, akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu waliopatiwa mikopo mbalimbali katika ghafla hiyo amesema mwanzoni hakua akijua kuwa watu wenye ulemavu wanaweza wakakopeshwa na serikali, lakini kupitia matangazo mbalimbali na hamasa iliyokuwa ikifanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi. Maryam Ukwaju aliweza kuhamasika na kufika ofisi za Halmashauri ambapo aliweza kupewa utaratibu ambao ulikuwa rahisi, usio na konakona yoyote na mara baada ya kukamilisha taratibu hizo amefurahi leo kukabidhiwa Bajaji yake. Ameahidi ya kwamba ataitunza vyema, na kutoa ajira kwa mtu mmoja atakaye endesha Bajaji hiyo na kumuingizia kipato ili aweze kurejesha mkopo huo na kuchukua mwingine.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.