Leo Alhamisi, tarehe 3 Novemba 2022 Mkuu wa mkoa wa Tanga Mh.Omari Tebweta Mgumba amehitimisha ziara ya siku mbili katika Halmashauri ya Mji Handeni aliyoianza tarehe 2 Novemba 2022 siku ya Jumatano. Katika ziara hiyo Mheshimiwa mkuu wa mkoa akiambatana na mwenyeji wake Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh.Siriel Mchembe ametembelea jumla ya miradi saba ya maendeleo na kufanya mikutano mitatu ya hadhara na wananchi wa Handeni Mjini.
Katika ziara hiyo Mh.Omari Mgumba alitembelea miradi ya maendeleo ifuatayo, kituo namba 15 cha mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki(EACOP) unaotokea Kabaale-Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania unaojengwa katika kata ya Mabanda Halmashauri ya Mji Handeni na mkandarasi mzawa kampuni ya SPEK, pia alitembelea ujenzi wa maabara za shule ya sekondari Misima kata ya Mabanda, ujenzi wa shule mpya ya msingi Bondo kata ya Kwamagome, ujenzi wa shule mpya ya sekondari Togeza kata ya Kwamagome. Miradi mingine aliyotembelea ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mlimani kata ya Mlimani, ujenzi wa kituo kipya cha afya Malezi kata ya Malezi na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mapinduzi kata ya Kwenjugo.
Akizungumza katika nyakati tofauti Mh.Omari Mgumba alishukuru, alipongeza, alielekeza na pia aliagiza mambo mbalimbali katika kuongeza ufanisi wa utoaji huduma wa serikali kwenda kwa wananchi, ambapo katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta alimshukuru mkandarasi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa vya uthaminishaji na utoaji fidia kwa wananchi walioondoka kwenye maeneo yao ili kupisha utekelezaji wa mradi huo, nae mkandarasi anaesimamia ujenzi huo Mhandisi Alnord Sililo alimueleza mkuu wa Mkoa ya kwamba mradi umefikia 48% na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 22 Disemba 2022, alieleza pia wakazi wa Mabanda na Misima wamenufaika moja kwa moja kutokana na ujenzi huo mahali hapo kwa kutatua changamoto ya uhaba wa maji ambapo visima viwili vya mradi huo vimekuwa vikihudumia wakazi wa eneo hilo na kuahidi kuwa mara baada ya mradi huo kukamilika visima hivyo vitakabidhiwa serikalini ili kuendelea kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo na maeneo ya jirani, vilevile watapatiwa mashamba mapya na kuelekezwa namna ya kulima kisasa.
Aidha Mh.Omari Mgumba alipotembela katika ujenzi wa maabara za shule ya sekondari Misima alipongeza baada ya kuridhishwa na hali ya mradi huo na kuwataka wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kusoma kwa bidii, pia alielekeza ujenzi wa uzio utakaounganisha jengo la bweni na vyoo vya wasichana ili kuimarisha usalama wa matumizi wa vyoo hivyo hususani kipindi cha usiku ambapo inawalazimu wanafunzi hao kushindwa kutumia vyoo hivyo ipasavyo kwa kuhofia usalama wao.
Akiwahutubia wananchi wa Bondo mtaa wa Kwaluwala, kata ya Kwamagome, Mheshimiwa mkuu wa mkoa amewapongeza wananchi hao kwa kujitoa kwao katika kujiletea maendeleo kwa kushirikiana na serikali katika ujenzi wa shule mpya ya msingi Bondo. Wakati huohuo amewasihi wakazi wa eneo hilo kuendelea kuvuta subira wakati serikali ikiendelea kufanyia kazi suala la mgogoro wa mipaka kati ya halmashauri ya Mji Handeni na halmashauri ya wilaya ya Kilindi ili kubaini eneo hilo kiutawala liko wapi, huku pia kukiwepo na taarifa inayosema eneo hilo ni msitu unaomilikiwa kihalali na Wakala wa Misitu Tanzania(TFS). Mheshimiwa mkuu wa mkoa amewaahidi wananchi hao mpaka kufikia tarehe 4 Novemba 2022 muafaka wa utatuzi wa migogoro hiyo utapatikana na watafahamishwa.
Katika ziara yake Mh. Omari Mgumba alitembelea ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mlimani na kuvutiwa na ubora wa majengo ya shule hiyo, hata hivyo amemuagiza Mhandisi wa halmashauri ya Mji Handeni, Benny Komba kukamilisha ujenzi huo kwa kufanya kazi usiku na mchana kwani licha ya ubora wa majengo hayo lakini ujenzi upo nyuma ya muda na ukamilike ndani ya wiki mbili na pia ameagiza kukamilisha utengenezaji wa thamani (meza na viti) vya shule hiyo kwa idadi iliyotolewa katika muongozo na kwa bajeti ya mradi huo.
Akiwa katika kituo kipya cha afya Malezi, Mheshimiwa mkuu wa mkoa ametoa pongezi juu ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi na kuanza kutumika kwa kituo hicho kitakachoondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma za afya ikiwemo kliniki ya mama na mtoto. Halikadhalika kituo hicho kinakwenda kuongeza idadi ya ajira mpya kwenye kada ya afya na nyinginezo.
Alipotembelea kata ya Kwenjugo mahali panapotekelezwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Mapinduzi kwa nguvu za wananchi Mheshimiwa mkuu wa mkoa ameagiza ujenzi wa shule hiyo uliokuwa unatekelezwa bila ya kufuata utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) usimame mara moja mpaka taratibu zitakapofuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa mkuu wa mkoa alihitimisha ziara hiyo kwa kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Mji wa Handeni katika mtaa wa Vibaoni, kata ya Vibaoni ambapo wananchi walipata fursa ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha za miradi mbalimbali katika Halmashauri yao na kumuomba Mkuu wa Mkoa kufikisha shukrani zao za dhati kwa mheshimiwa Rais, pia walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali, yaliyotolewa majibu na mheshimiwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mwenyekiti wa halmashauri Mh. Mussa Mkombati(Diwani CCM) na mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Handeni, Mh. Maryam Ukwaju.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa kwa kuahidi kuanza kuyafanyia kazi mara moja.
Mheshimiwa mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake kwa kuwapongeza viongozi wa chama na serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi wa halmashauri ya Mji Handeni, kwa kudumisha amani na kutoa ushirikiano kikamilifu katika ziara yake ya kikazi ya muda wa siku mbili.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.