Leo Alhamisi, tarehe 1 Desemba 2022 maadhimisho ya siku ya UKIMWI yamefanyika katika kituo cha Afya Malezi kilichopo Halmashauri ya Mji Handeni kata ya Malezi. Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wamehudhuria katika maadhimisho hayo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Bi.Siriel Mchembe.Katika maadhimisho hayo viongozi pamoja na wananchi wamejitokeza kupima kwa hiari VVU, kutambua hali zao za kiafya na kutoa ushirikiano wa juhudi za serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe amewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na matumizi ya pamoja kwa vitu vyenye ncha kali hususani kwenye maeneo wanapopata huduma za saloon kwani vifaa vinavyotumika kutolea huduma ni vyenye ncha kali hivyo visipotumika ipasavyo na kutochemshwa vitapelekea kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI .
Wakati huohuo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni Mh.Mussa Mkombati(Diwani CCM) amewataka wananchi kujitokeza kupima virusi vya UKIMWI pale wanapopata nafasi ya kufanya hivyo na kuwahakikishia kuwa huduma hii inapatikana kwa wakati kwa kila anayestahili.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bi.Maryam Ukwaju amewataka wananchi kushirikiana na kutowanyanyapaa waathirika wa VVU na pia walioathirika wasijinyanyapae ili kuweka usawa katika jamii kwani kutambua Afya yako ni namna nzuri ya kuweza kuishi kwa matumaini na kutimiza malengo yako.
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi, mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Joyce Gidion amesema maambukizi ya VVU katika Halmashauri ya Mji Handeni yamepungua ambapo mpaka kufikia Oktoba 2022 idadi ya waliojitokeza kupima VVU ni jumla ya wananchi 9,453 kati yao wanaume ni 4,447 na wanawake ni 5,006 na kugundua walioathirika kuwa na idadi ya 365 wanaume wakiwa ni 164 sawa na 4% na wanawake ni 201 sawa na 3.7% ameeleza pia jumla ya wateja 2,600 wamepatiwa dawa za kufubaza VVU, 830 wakiwa ni wanaume na 1,770 ni wanawake.
Katika nyakati tofauti wananchi wameeleza changamoto zinazowapelekea kutojitokeza kwenye upimaji wa VVU moja wapo ni baadhi ya wananchi katika jamii kunyanyapaa waathirika wa VVU na kupelekea ukosefu wa usawa katika jamii, pia wameishukuru serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI kwa jitihada za kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kwa kuwapatia elimu kuhusu VVU katika vituo vya kutolea huduma za Afya, kinga za kuzuia maambukizi mapya na kutoa dawa kwa waathirika wa VVU.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.