Mkuu wa wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe ameongoza zoezi la ugawaji wa pembejeo na viuatilifu vya kilimo cha zao la korosho katika kata ya Vibaoni Mtaa wa Vibaoni Kati Halmashauri ya mji Handeni kwenye moja ya shamba la mfugaji na mkulima wa korosho Dkt.Raynold Mlinga.
Aidha kwenye zoezi hilo amemuagiza Afisa Kilimo kuunda mara moja AMCOS ili wakulima wapate soko na bei ya kueleweka ya zao la korosho ili kuepusha wakulima kuuza mazao yao kwa wanunuzi binafsi(vishoka) wa zao hilo la korosho na kupata adha ya kufuata soko la korosho (AMCOS) lililopo Mkata badala ya soko kumfuata mkulima kwa ajili ya manunuzi.
Pia Mh. Mkuu wa wilaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi. Maryam Ukwaju kuhakikisha kuwa maafisa ugani wanakuwa na jukumu moja tu mbali na kukaimu katika nafasi nyengine za utendaji wa mitaa, lengo likiwa kuimarisha na kufikia maendeleo ya zao la kimkakati la korosho kwa kuweza kupata muda mrefu kwa ajili ya kuwahudumia na kushirikiana na wakulima katika maeneo yao husika na kuepusha kukosekana huduma ya maafisa hao pindi panapokuwa na majukumu mengine ya kiutendaji.
Vilevile amemuagiza Afisa Kilimo pamoja na kila afisa ugani kuwa na shamba darasa kwa ajili ya kuelimisha wakulima na kuwaonyesha namna bora juu ya kilimo cha zao hilo, kuhamasisha wakulima juu ya zao la korosho na namna linavyoweza kuinua hali ya kiuchumi ya mkulima, kugundua changamoto zitokanazo na wadudu na upungufu wa pembejeo na kutambua mazao yenye ustawi mzuri katika eneo hilo kwa kupanda aina tofauti za mazao ili kuwaelekeza namna bora ya kilimo cha zao hilo.
Katika zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe amewataka wakulima wote wajisajili katika daftari la wakulima katika mfumo wa kielektroniki ili wapate nafasi yakutambulika, kuelimishwa na kusaidiwa katika mbinu bora za kilimo.
Wakati huohuo amempongeza Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bi Aldegunda Matunda kwa kuweza kuongeza idadi ya miche ya zao hilo la kimkakati na kufikia idadi ya miche elfu kumi na tano(15,000) na kuweka malengo ya uzalishaji wa korosho kutoka tani 2.2 hadi tani 15.3 sawa na hekari 308 hadi hekari 1080 kwa mwaka wa kilimo 2022/23 na kumtaka asimamie utekelezaji wa malengo hayo, pia amewasisitiza wakulima kupanda miche mingi zaidi ya zao la korosho ili kuweza kuepukana na mashamba pori.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Sekta ya Kilimo na kuipa nguvu maradufu ili kupiga vita maadui watatu wa taifa yaani ujinga, umaskini na maradhi ambapo mkulima akiinuka kiuchumi ataweza kuepukana na umasikini, maradhi kwa kukata bima ya afya itakayompatia matibabu na ataweza kusomesha watoto ili waepukane na ujinga.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.