Leo Ijumaa ya tarehe 14 Julai 2023, Shirika la WaterAid Tanzania limeikabidhi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(HTM) bwawa la Maji, lilokuwepo Halmashauri ya Mji Handeni, mtaa wa Kampene katika kata ya Kideleko. Hafla ya makabidhiano hayo imehudhuriwa na Mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Maji Mhe.Maryprisca Mahundi.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe.Maryprisca Mahundi, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada anazozifanya katika kuboresha sekta ya maji katika Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Vilevile amempongeza Mkuu wa wilaya Mhe.Alberto Msando kwa Kushirikiana na Mamlaka ya maji vijijini(RUWASA) katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo. Pia amempongeza Mbunge wa Jimbo la Handeni Mji Mhe.Reuben Kwagilwa kwa kutafuta wafadhili ambao wamekuja kuleta tija katika kuwezesha jamii kupata huduma karibu na makazi yao.
Mhe.Maryprisca Mahundi, ameishukuru kampuni ya Serengeti Breweries(SBL) kwa kufadhili mradi huo kwa fedha za Tanzania shilingi milioni 380 ambazo ni zaidi ya asilimia tisini (90%) za gharama ya mradi huo, ambao umesimamiwa na shirika la WaterAid.
Mkurugenzi mkazi wa shirika la WaterAid Tanzania Bi. Anna Mzinga, akisoma ripoti ya utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kwamaizi mbele ya mgeni rasmi. Pichani wa pili kushoto ni Mhe.Maryprisca Mahundi Naibu Waziri wa maji, wa kwanza kushoto Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh. Alberto Msando, Mbunge wa Handeni Mji Mhe.Reuben Kwagilwa wa Pili kulia na Mkurugenzi wa Halmashauri Bi.Maryam Ukwaju wa kwanza kulia
Nae Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe.Alberto Msando amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa maji katika wilaya ya Handeni kufika 40.6% kutoka asilimia 38% kama ilivyokuwa katika mwaka 2020/21, kwa kipindi kifupi alichokuwa madarakani. Ambapo Halmashauri ya Mji Handeni imekuwa na 42% za upatikanaji wa maji. Pia Mkuu wa wilaya ameahidi kuwa hakutakuwa na shilingi itakayopotea katika utekelezaji wa miradi , ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii kwa zaidi ya 85% kabla ya mwaka 2025.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju, akipokea cheti cha kutambuliwa kutoka kwa Naibu waziri wa Maji Mhe.Maryprisca Mahundi, kilichotolewa na Shirika la bia la Serengeti(SBL), katika hafla ya kukabidhi Bwawa la Kwamaizi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(HTM)
Mhe.Reuben Kwagilwa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo, ambapo wameweza kuleta mitambo kwenye utekelezaji wa mradi huo na kupunguza gharama ambazo zingehitajika kwa ajili ya kukodisha mitambo hiyo, Mhe.Kwagilwa amewataka wananchi kutunza mazingira na vyanzo vya maji pamoja na mradi huo, kwa kutofanya shughuli za makazi na uchumi kwa umbali wa mita 60 kutoka kwenye bwawa hilo, kwa kuwa mradi huo umetekelezwa kwa kuzingatia sheria za maji.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.