Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli ameahidi kumaliza kero ya upatikanaji wa Maji ya uhakika kwa Wananchi wa Handeni.
Ametoa ahadi hiyo leo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Handeni eneo la viwanja vya Kwambwembwele Handeni Mjini akitokea Tanga kwenye uwekaji wa jiwe la Msingi wa Bomba la mafuta linalounganisha Tanzania na Uganda.Amewaeleza Wananchi kuwa atahakikisha tatizo la Maji Handeni linatatuliwa kwa sababu kuna miradi mitatu ambayo inatarajiwa kuleta matokeo chanya ikiwemo mradi wa Bilioni 2.6 unaomalizikia utakaounganisha Maji maeneo ya Manga,Mkata na Handeni,mradi wa zaidi ya Bilion 200 Maji yatatolewa Mto pangani hivyo kumaliza tatizo la Maji.
Amewataka wakandarasi waliopo na wajao kufanya kazi kwa weledi na wakati ili kufikia malengo kwa wakati uliopangwa na kwamba hatakuwa tayari kuwavumilia wakandarasi watakaokwamisha upatikanaji wa Maji ya uhakika Handeni."Wakandarasi mliopo na mtakaokuja mkitaka kugombana na mimi chezeni na miradi hii Maji Handeni" amesema Rais Dkt.John Magufuli.
Kwa upande mwingine amewataka Wananchi wa Handeni kuwa wavumilivu na kushirikiana vyema na watumishi wa kada ya Afya kwa sababu wanafanya kazi kubwa ya kuwahudumia Wagonjwa kulinganisha na idadi ndogo ya watumishi iliyopo,amewaeleza kuwa ajira zilisitishwa kwa muda kutokana na zoezi la uhakiki hivi punde watumishi wa Afya wataongezeka kwani kibali cha ajira kimekwishatolewa .Aidha amewataka Wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kuboresha huduma za Afya na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati pindi wanapohitaji kuhudumiwa.
Mwisho amepongeza Wananchi wa Handeni kwa namna wanavyojishughulisha na shughuli za kiuchumi hususani kilimo na ufugaji ambazo ni tija kwa maendeleo ya Taifa letu na kuwataka kuendelea na motisha ya kufanya kazi kwa juhudi huku wakiendelea kulinda na kuitunza Amani na Umoja wetu uliopo ili kuendeleza Taifa.Rais pia ameahidi kumalizia barabara inayounganisha Dumila na Handeni yenye urefu wa km 50 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na usafirishaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amezungumza na Wananchi wa Handeni alipokuwa akimalizia ziara yake akitokea Tanga Mjini
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.