Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, Mhe. Mussa Mkombati, ameongoza hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Bwawa la Kwamaizi. Hafla hii ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo na wakazi wa Kata ya Kideleko.
Katika hotuba yake, Mhe. Mkombati ametoa shukrani kwa wadau wa maendeleo ambao Water Aid, OKF, HTM na Serengeti Breweries kwa kusaidia kufanikisha mradi huu wa usambazaji wa Maji kwa wananchi wa kata ya Kideleko.
Pia ametoa shukrani na pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira wezeshi yanayowavutia wadau kushiriki katika miradi ya Maendeleo.
Mwenyekiti amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kutekeleza mradi huu wa usambazaji maji na kuwataka wananchi kulinda vifaa vya mradi vitakavyofika ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati.
Pia amekumbusha umuhimu wa kujenga vyoo bora kama njia ya kulinda vyanzo vya maji, hasa katika kipindi cha mvua. Aidha Mhe. Mkombati amesisitiza kuwa mafanikio ya awamu ya kwanza ya Mradi huu ni matokeo ya ushirikiano mkubwa wa wadau wote, lakini bado chanzo hiki cha maji kipo mbali na makazi ya wananchi, hivyo hitaji la miundombinu ya kuwafikishia maji karibu na makazi yao linabaki kuwa muhimu.
Katika awamu ya pili ya mradi, changamoto ya umbali wa chanzo cha maji na makazi ya wananchi itapunguzwa kwa kujenga miundombinu ya mabomba ya maji yenye urefu wa kilomita 3.5, tanki la kuhifadhia maji lita 100,000, chujio la kutibu maji, na vituo vitatu vya kuchotea maji vyenye mita za malipo. Pia, serikali itaongeza vituo zaidi vya maji kulingana na mahitaji ya jamii. Utekelezaji wa mradi huu pia utahusisha mafunzo na kampeni za usafi na uhifadhi wa mazingira kwa jamii, kuhakikisha matumizi endelevu ya maji na mazingira bora.
Mradi huu wa awamu ya pili umefadhiliwa na Operakallaren Foundation (OKF), iliyochangia shilingi milioni 359,633,851, huku serikali na wananchi wakitoa mchango wa vitendea kazi na nguvu kazi ili kufanikisha utekelezaji wa mradi kwa wakati.
Aidha, Katibu Tarafa wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bi Julieth Mushi, alitoa shukrani kwa Water Aid na wadau wa maendeleo kwa kutekeleza mradi huu wa maji, akibainisha kuwa ni hatua kubwa inayosaidia kumtua mama ndoo kichwani na kuleta unafuu kwa wakazi wa eneo hilo.
Afisa Mazingira wa Halmashauri, Bwana Toba Mhina, alizungumzia umuhimu wa kupanda miti rafiki wa maji ili kulinda bwawa na kuimarisha uhifadhi wa maji, akieleza kuwa miti hiyo itasaidia pia katika kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Nae Diwani wa Kata ya Kideleko aliwashukuru Water Aid na OKF kwa kuleta mradi huu karibu na jamii na kuahidi ushirikiano kwa wadau wote waliofadhili mradi huu. Aliwahimiza wakazi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi na alisisitiza kuwa mradi huu utaleta faida ya muda mrefu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.