Leo Jumamosi Tarehe 04/03/2023 Halmashauri ya Mji Handeni imehitimisha mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo wa kielektroniki wa malipo (FFARS) kwa walimu wa shule za msingi na sekondari. Katika mafunzo hayo mada mbalimbali zilifundishwa, ikiwemo namna ya kufanya uambatanishaji wa nakala za malipo, pamoja na namna ya kutumia mfumo huo. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Handeni yamehudhuriwa na walimu wakuu, wahasibu, mweka hazina na maafisa elimu msingi na sekondari.
Walimu wakisikiliza kwa umakini mada katika mafunzo ya mfumo wa FFARS yaliyofanyika Halmashauri ya Mji Handeni
Katika semina hiyo Mhasibu wa Halmashauri ya Mji Handeni, ndugu John Sarus amewataka walimu wanaosimamia miradi na manunuzi ya vifaa mbalimbali vya shule, kuweka nyaraka zote muhimu pamoja na kuzitunza kwenye kabrasha husika na kupangilia katika taratibu maalum.
Nae Mkuu wa shule ya msingi Mapinduzi, ndugu Robert Njama amesema mafunzo ya FFARS na utunzaji wa nyaraka yamesaidia kufahamu mpangilio, utunzaji wa nyaraka za serikali na hati mbalimbali za malipo, ameahidi kutokana na maelekezo yaliyotolewa na wataalam kutoka ofisi ya fedha, yeye kama msimamizi wa taasisi kuwa taratibu zote zitafuatwa ili kuepusha hoja ya taarifa juu ya malipo, wakati wa ukaguzi katika kipindi cha kila robo.
Mhasibu wa Halmashauri ya Mji Handeni, ndugu John Sarus akifafanua jambo,katika mafunzo ya mfumo wa FFARS uliofanyika Halmashauri ya Mji Handeni
Kwa wakati huohuo mkuu wa shule ya sekondari Kwenjugo, mwalimu Juma Abdurabi amesema kulikuwa na changamoto ya namna ya kupangilia nyaraka, kwenye kabrasha ambazo zilipelekea kuwa na hoja, wakati wa kupitia malipo ya kila robo. Na hatimaye kutokana na mafunzo haya yamesaidia kupata ufahamu, juu ya taratibu sahihi za kupangilia nyaraka hizo, pia ameishukuru Halmashauri ya Mji Handeni kwa kuendesha mafunzo hayo, ambapo yameweza kuwasaidia watumiaji wapya wa mfumo, kuufahamu na kujua namna ya kuutumia.
Kwa upande wake mwalimu wa fedha shule ya msingi Azimio Mwalimu.Agness Raphael amemshukuru Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dokta. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha walimu kwa kuwapatia vishikwambi, ambavyo vimekuja kutatua changamoto ya uhaba wa vifaa, hivyo wameweza kutumia mifumo mbalimbali kwa urahisi kutokana na vishikwambi hivyo.
Walimu wakiendelea kupatiwa mafunzo ya mfumo wa FFARS, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Handeni
Hata hivo Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Handeni, ndugu Mpakani Kassim amesema kuwa mafunzo yameenda vizuri na yameeleweka, mafunzo hayo yataongeza umakini kwenye utunzaji wa kumbukumbu za hati ya malipo. Na yamekuwa ni mafunzo yaliyowezeshwa kwa ajili ya kukumbusha, namna sahihi za kufanya malipo na manunuzi ya vifaa mbalimbali vya shule kupitia mfumo, ukizingatia kuwa kuna maboresho yalifanyika juu ya mfumo huo siku za hivi karibuni, pia amewataka walimu waliohudhuria, kuzingatia mafunzo hayo ili kuhakikisha kuwa, wanayafanyia kazi mafunzo hayo na wanapata uzoefu.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi. Maryam Ukwaju amewaagiza walimu wa fedha wa shule zote, kuwa ndani ya wiki moja mpaka kufikia tarehe 10/03/2023 wawe wamekamilisha upangaji wa nyaraka zote za malipo za kuanzia mwezi Julai 2022 mpaka mwezi Februari 2023, kuzihakiki, kukamilisha bank reconciliation na kupitiwa pamoja na kuziwasilisha ili zipate kuhakikiwa na wahasibu wa Halmashauri
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.