WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona mabadiliko kwenye sekta ya mifugo si tu kwa kijiji cha Msomera bali kwa nchi nzima.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 7, 2023) wakati akizungumza na viongozi na wananchi waliohudhuria kikao cha siku moja alichokiitisha wilayani Handeni, mkoani Tanga ili kukabidhi rasmi mradi wa makazi maalum katika kijiji cha Msomera kwa Wilaya za Handeni na Kilindi.
"Serikali hii imesema eneo la Msomera litakuwa eneo la mfano kwa ufugaji wa kisasa na wa kibiashara. Kwa hiyo ni lazima tuweke utaratibu wa kufanya lionekane ni eneo la ufugaji wa kisasa," amesema.
Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni kwa sasa ni makazi ya wananchi ambao kuanzia Juni, 2022 walihama kwa hiyari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika eneo hilo. Mara baada ya kuwasili, walipewa nyumba za kuishi za ukubwa wa vyumba vitatu kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2.5 na jingine la malisho la ekari tano.
Ameziagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Mifugo ziweke utaratibu utakaowafanya wafugaji wafuge kitaalamu badala ya utaratibu wa mtu kuwa na mifugo mingi halafu anashindwa kuihudumia kwani utaratibu huo hauna tija.
"Wizara ya Mifugo pamoja na Ofisi ya Rais - TAMISEMI tengenezeni taratibu za kuonesha mfugaji wa Msomera mwenye ng'ombe 70 anafuga kwa tija zaidi kuliko mwenye ng'ombe 300. Hii inaweza kutumika hata kwenye mikoa mingine ambako kuna wafugaji," amesisitiza.
Amezitaka Halmashauri za Mji Handeni na Wilaya za Handeni na Kilindi zinapoandaa bajeti zao kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, zihakikishe zinaingiza mahitaji ya uendelezaji huduma kwenye kijiji cha Msomera ili kuimarisha ustawi wa wananchi wa kijiji hicho.
Pia amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wanapoenda kufanya ziara kwenye kijiji hicho wahakikishe wanaanzia kwanza kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kujitambulisha rasmi ndipo wapatiwe maafisa wa kuongozana nao.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.