Leo Jumanne tarehe 25/04/2023 Halmashauri ya Mji Handeni, imezindua rasmi wiki ya chanjo duniani ya mwaka 2023 yenye Kauli mbiu ”Tuwafikie wote kwa chanjo” na ujumbe ”jamii iliyopata chanjo, jamii yenye afya”. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika katika kata ya Mabanda, kwenye Zahanati ya Misima. Ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Mji Handeni, watumishi wa Idara ya Afya na wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kupata chanjo na elimu juu ya chanjo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Handeni Dokta.Feisal Said, akiongea na wananchi waliohudhuria katika ghafla ya uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani, uliofanyika katika kata ya Mabanda, Zahanati ya Misima
Akizungumza katika ghafla hiyo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Handeni Dokta.Feisal Said, amewafahamisha wananchi juu ya umuhimu wa chanjo, ambao ni kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayoweza kupelekea vifo au ulemavu, hivyo kutokana na chanjo hizo na kuzingatia ukamilishaji wa dozi za chanjo wanaweza kuepukana na magonjwa hayo. Katika ghafla hiyo wazazi wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano wamesisitizwa kuwapeleka watoto hao kwa ajili ya kupata chanjo na kuwakumbusha wote ambao hawakupata chanjo ya UVIKO 19 kufika katika vituo husika kwa ajili ya kupata chanjo hiyo. Katika Halmashauri ya Mji Handeni, chanjo hizi zinatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na shule ambazo zitatembelewa na kutolewa chanjo za kukinga saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti wa kuanzia umri wa miaka 14.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni Mhe.Mussa Mkombati, akiongea na wananchi waliohudhuria katika uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani, uliofanyika katika kata ya Mabanda, Zahanati ya Misima
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni Mhe.Mussa Mkombati, amefurahishwa na mahudhurio ya wazazi waloijitokeza kuwaleta watoto kwa ajili ya kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, amempongeza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Handeni Dokta.Feisal Said, kwa kufanya zoezi la chanjo kwa asilimia 112 katika mwaka 2022 na amewasisitiza kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji Handeni, katika ghafla hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni aliendelea kusema kuwa kwa wale wote ambao hawajapata chanjo ya UVIKO 19, wajitokeze ili kuepukana na maradhi yanayopelekea kushindwa kupumua kwa urahisi na hatimaye kupelekea gharama kubwa ya matibabu yake. Akihitimisha Mhe.Mussa Mkombati, amewasisitiza wazazi juu ya kuwasimamia watoto katika malezi yenye maadili mema ili kuepukana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Handeni waliohudhuria katika uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani, uliofanyika katika kata ya Mabanda, Zahanati ya Misima
Nae Bi.Esther Laizer mkazi wa kata ya Mabanda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwajali wananchi wake, kuwatatulia changamoto za vifaa na kuwasogezea huduma mbalimbali za jamii karibu na makazi yao, ikiwemo huduma ya afya ambapo kwa sasa wanaweza kupata huduma hizo bila kulazimika Kwenda umbali mrefu.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.