Leo tarehe 12/11/2022 Halmashauri ya Mji Handeni imeanza rasmi kuuza mahindi ya bei nafuu kwa wakulima wa Halmashauri ya Mji Handeni katika ghala la ndugu Hafidhi linalopatikana maeneo ya njiapanda ya Kwabaya, kufuatia na uhaba na kuchelewa kwa msimu wa mvua kwa kipindi kirefu iliyopelekewa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha upungufu wa chakula na kupanda kwa bei ya mazao ya chakula kwa wakulima, kufuatia hali hiyo serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inahakikisha wananchi wanaendelea kupata chakula kwa kusambaza mahindi yanayopatikana kwa bei nafuu. Mahindi hayo yanauzwa kwa bei ya shilingi 898/= kwa kilogram moja ambapo kila kaya inaweza kununua mahindi hadi Kilogram zisizozidi 100.
Katika nyakati tofauti wananchi wa Halmashauri ya Handeni Mji wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea chakula hicho katika maeneo yao kwa bei nafuu kulinganisha na bei ya wafanya biashara wa kawaida wanaouza chakula hicho kwa bei ya shilingi 1,300/= kwa kilogram na kupelekea kushindwa kupata chakula cha kutosha kwa mahitaji ya wananchi hususani kwa wananchi walio katika hali ngumu ya kiuchumi na wanufaika wa mfuko wa kusaidia kaya maskini TASAF.
Aidha Mtendaji Kata wa Kata ya Kideleko Bi.Asia Mussa Kasopa amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe kwa kuhakikisha kuwa mahindi hayo yanauzwa katika eneo ambalo ni rahisi kwa kila mwananchi kufika ili kuweza kununua mahindi hayo na kuhakikisha kuwa mahindi hayo yanauzwa kwa ajili ya chakula tu na si vinginevyo, Bi.Asia Kasopa amewashauri wananchi wote kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kununua mahindi kwani mahindi yapo kwa kiwango kikubwa na cha kutosha kwa kila mwananchi mwenye uhitaji wa chakula hicho.
Kwa upande wake Mhasibu msaidizi wa NRFA Dar-es-salaam Bi.Valeria Mwenda ameeleza kuwa zoezi la ununuzi limepokelewa kwa muitikio mkubwa sana na idadi ya kaya 44 zimefanikiwa kununua mahindi kwa siku ya kwanza ya zoezi hilo, kati ya kilogram 5 kwa kiwango cha chini mpaka kilogram 100 ambacho ni kiwango cha juu kabisa cha manunuzi ya mahindi kwa kaya moja na jumla ya tani 2.229 sawa na wastani wa kilogramu 50.659 kwa kaya, pia amewasisitiza watendaji kata/mitaa wawapatie utaratibu na kuwafahamisha bei elekezi ya kununua mahindi hayo ili kuepusha adha ya wakulima kufika eneo la manunuzi na kushindwa kufanya manunuzi kwa kukosa vigezo vya manunuzi ikiwemo kutokuwa na barua ya utambulisho na kuwalazimu kurudi kwenye uongozi husika na kupata barua za utambulisho, pia Bi.Valeria Mwenda amewakumbusha wananchi kuwa wanunuzi wote lazima wawasilishe barua zao za utambulisho kutoka kwenye uongozi wao wa kata/mitaa pindi wanapokuja kufanya manunuzi ili kuepusha udanganyifu na kuuza mahindi kwa matumizi ambayo sio ya chakula.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Bi.Maryam Ukwaju anaendelea kuwakaribisha wananchi na wakazi wote wa Halmashauri ya Mji Handeni kwenye ununuzi wa mahindi ya bei nafuu unaoendelea katika ghala la ndugu Hafidhi linalopatikana maeneo ya njiapanda ya Kwabaya.
Abdulkadir Kassim
Handeni Mji.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.