Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni Mh.Mussa Abeid Mkombati(Diwani) leo Jumapili ya tarehe 30-04-2023 ameanza ziara ya kutembelea nyumba za ibada na taasisi za elimu ikiwa ni utekelezaji wa azimio la baraza la waheshimiwa madiwani lilofanyika siku mbili zilizopita.
Akiwa katika ziara hiyo, Mh.Mkombati amewaomba viongozi wa dini kuliombea taifa ili Mwenyezi Mungu aweze kuliepusha taifa hili dhidi ya mmomonyoko wa kimaadili hususani suala zima la ushoga na ndoa za jinsia moja.
Akizungumzia kuhusu ukatili wa kijinsia kwa watoto, Mh.Mkombati amewasihi waumini hao kuzungumza na watoto wao juu ya uthamani wa miili yao na pindi mtu akitaka kuwashika maeneo ya kifua, sehemu za siri na kwenye makalio wakatae kwa kusema “SITAKI” na wawaambie watoto hao kutoa taarifa kwao wazazi bila woga, nao wazazi wapatapo taarifa hizo wachukue hatua haraka ya kutoa taarifa polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
“Inasikitisha kuona ndani ya Handeni, leo hii wapo wazazi ambao wanawabaka na kuwalawiti watoto wanaowalea wenyewe. Niwaombe sana waumini, siwakatazi kuwapokea wageni kwenye nyumba zenu, lakini mgeni anapofika nyumbani kwako, na una watoto wadogo, chukua watoto wako lala nao mwenyewe. Ndugu zangu, taarifa nyingi zinaonyesha watoto wetu wanaharibiwa na watu wetu wa karibu ambao huwezi hata kuwafikiria vibaya. Tujihadhari sana” alisisitiza
Ziara hii ya Mheshimiwa Mkombati iliyoanza saa 12 asubuhi imefanikiwa kutembelea zaidi ya makanisa 7 kwa siku ya leo na itaendelea kwenye nyumba za ibada nyingine katika siku za hivi karibuni.
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.