Mradi wa ujenzi wa bwawa la Kwamaizi uliopo mtaa wa Kwamaizi, kata ya Kideleleko, Halmashauri ya Mji Handeni ulioanza kujengwa mwezi februari mwaka huu ambao unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 380 utakapokamilika, fedha zilizotolewa na kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited, umefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa tano.
Akizungumza katika hafla ya utoaji vyeti kwa wahitimu wanawake 24 wanaounda Kikundi Cha Maendeleo cha Kata ya Kideleko, Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Bi.Rispa Hatibu amesema bwawa hilo litakapokamilika linatarajiwa kuwa na ukubwa wa mita za ujazo 135 na kuhifadhi maji ya kuwatosheleza zaidi ya wakazi 2000 wa eneo la mtaa wa Kwamaizi pamoja na maeneo ya jirani.
“Tunao washirika wetu katika huu mradi ambao ni WaterAID, wao wanasimamia usalama wa huu mradi lakini niwaombe wananchi wa Kwamaizi na wote watakaonufaika na huu mradi, tunzeni chanzo hiki cha maji”alisisitiza
Mkuu wa Miradi kutoka WaterAID Dkt. Happiness Wilbroad amesema shirika lao kwa zaidi ya miaka 40 limekuwa likitekeleza miradi ya kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa jamii, na katika kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu jamii hushirikishwa katika utekelezaji wa miradi, na katika ujenzi wa bwawa la Kwamaizi, kikundi cha wanawake 24 wa Kwamaizi wamepewa mafunzo ya utunzaji mazingira kulizunguka bwawa pamoja na mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo utengenezaji wa sabuni za maji.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Wakili Albert G. Msando ametoa shukrani kwa uongozi wa kampuni ya bia ya Serengeti, kwa ufadhili wa mradi huo lakini pia kwa usimamizi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Halikadhalika, amewapongeza shirika la WaterAID kwa usimamizi wao wa karibu na uratibu tangu mradi unaanza hadi sasa.
Pia, aliishukuru ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni kwa ushirikiano wa karibu inaoutoa, akitolea mfano mafunzo ya kikundi cha wanawake 24 kuratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii. Kuhusu kikundi cha wanawake, amewataka wakawe mabalozi wazuri juu ya utunzaji wa mazingira katika bwawa mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo ambayo leo hii wamehitimu na kukabidhiwa vyeti
Barabara ya Korogwe - Handeni
Anuani ya Posta: S.L.P 51 HANDENI
Simu ya Mezani: 027-2641807
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: td@handenitc.go.tz
Copyright ©2022 GWF . All rights reserved.